UMOJA WA MUNGU

Kuna Mungu mmoja wa kweli.  Huyu Mungu mmoja na wa kweli yu aishi milele,  ni wa milele, mwenye nguvu zote (mwenyezi au mwenye nguvu zisizo na kikomo) aliyeenea pote  (yupo kila mahali kwa wakati mmoja), anayefahamu yote (ajuaye yote au mwenye ujuzi usio na kikomo), mtakatifu kwa asili,  kusudi, tabia na Uungu. Umoja wa Mungu ni msingi wa Biblia na mafundisho yote ya Ki-biblia.

     Musa anapowakumbusha watu wa Mungu kuzishika amri zake, katika kumbukumbu la torati 6:4 anatangaza Kumbukumbu la Torati 6:4-5

“Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. 

Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.”  Hii amri ya kwanza na iliyo kuu! 

Yesu alisibitisha ukweli huu wa Agano la Kale kwenye maandishi ya Agano jipya ya Marko 12:29-30,  “Yesu akamjibu, ya kwanza ndiyo hii, sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja….”

 Katika   Isaya   44:6,  Mungu  mwenyewe anasema, 

Isaya 44:6  “BWANA, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, BWANA wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu.”

   Kwa kanisa lililoko Galatia, Mtume Paulo ameandika, “Mungu ni mmoja” (Galatia 3:20). Kwa kanisa lililoko Efeso, Mtume Paulo ameandika,  “Bwana mmoja, Imani moja, Ubatizo mmoja, Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote” (waefeso 4:5-6).

DHIHIRISHO, OFISI, VYEO VYA MUNGU

Huyu Mungu mmoja wa kweli alijidhiirisha  katika njia nyingi tofauti, akitumia ofisi tofauti na vyeo vingi.

Kama vile Paulo anavyosema, (1 Timotheo 3:16)

“Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu:  Mungu

alidhihirishwa katika mwili, akajulikana kuwa na haki katika Roho, akaonekana na

malaika, akahubiriwa katika Mataifa, akaaminiwa katika ulimwengu, akachukuliwa juu katika utukufu”                 .

       Yohana 4:24 anasema,“Mungu ni roho…” (Umoja siyo wingi). Baba na Roho Mtakatifu ni vyeo tu vya Roho wa Mungu, anayekaa ndani ya Mwana (Yesu Kristo),

udhihiriko wa Mungu katika mwili. Ikiwa wakati wote tutakumbuka kuwa neno Baba, linapotumika kwa kumtaja Mungu, linamaanisha Roho wa Mungu!

Mungu alitumia ofisi ya Baba katika Uumbaji -Mungu kwa Mwanadamu.

Malaki 2:10 anaeleza, “je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu?” Waefeso 4:6 anasema “Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote…”

Mungu alitumia ofisi ya Mwana katika Ukombozi- Mungu pamoja na Mwanadamu. Mathayo 1:21 anasema,

“Naye atazaa mwana, nawe utamwita Jina Lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.”

Mathayo 1:23 anasema, “Tazama bikira atachukua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli, yaani, Mungu pamoia nasi.”

Mungu alitumia ofisi ya Roho Mtakatifu katika Uzao Mpya -Mungu ndani ya Mwanadamu.

Yohana 1:12-13 hututia moyo, “Bali wote waliompokea Aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” 

Tito 3:5 anasema,“…kwa kuoshwa, kwa kuzaliwa kwa pili, na kufanywa upya na Roho Mtakatifu.”

Kwa hiyo, Roho wa Mungu (Umoja siyo Wingi), aliitwa kwa cheo cha Baba, Roho huyo huyo wa Mungu Akaitwa kwa cheo cha Roho Mtakatifu na Roho, huyo huyo wa Mungu Akauvaa mwili wa mwanadamu akitumia cheo cha Mwana. Hata hivyo, palikuwepo na Roho Mmoja tu wa Mungu na Nafsi Moja tu ya Mungu.

Huyu Roho Mmoja Alikuwa ndani ya Mtu huyu Mmoja, mwanadamu Kristo Yesu!

2 Wakorintho 5:19 inathibitisha jambo hili kwa kusema, “Yaani, Mungu Alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na

nafsi yake…” (nafsi yake siyo nafsi zao). Jambo hili liko wazi sana na dhahiri katika maandiko hakuna nafsi 3 za Mungu, ni moja tu na Jina Lake ni Yesu!

AGANO LA KALE HUFUNDISHA KUNA

MUNGU MMOJATU

        Maneno yenye ufasaha zaidi ya fundisho la Mungu mmoja yanapatikana katika Kumbukumbu la Torati 6:4, 

“Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja.”

Mstari huu wa Biblia ni wa pekee zaidi na tamko lenye umuhimu katika imani ya Kiyahudi. Katika Isaya yote,Bwana Mungu kwa usahihi kabisa ametangaza Umoja Wake kwa kurudia rudia!

“Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni BWANA, zaidi yangu mimi hapana mwokozi” (lsaya 43:10-11). “..Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu” (Isaya 44:6). Kama kungekuwa na utatu au nafsi 3 za Mungu, zote za milele na au zinazolingana, basi andiko lingesema “Sisi ni wa kwanza, na sisi ni wa mwisho; zaidi yetu sisi hapana Miungu.

“..Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi?hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine” (Isaya 44:8).

“..Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoia nami?” (lsaya 44:24) “..

Hapana mwingine zaidi ya mimi; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine”(lsaya 45:6).

Kama wako watatu, ni kwa nini Bwana anawakana hawa wengine wawili? Hapana watatu, ni mmoja tu! wala hapana Mungu zaidi ya Mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi,mkaokolewe, enyi nchi zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine “(Isaya 45;21-22).

       “Kumbukeni mambo ya zamani za kale;maana mimi ni Mungu,wala hapana mwingine;mimi ni Mungu,wala hapana aliye kama mimi:” (Isaya 46:9).

“..Wala sitampa mwingine utukufu wangu:” (Isaya 48:11). “….Utukufu wangu sitampa mwingine…” (Isaya 42:8).

“Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi” Isaya 37:16).

“Je sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? (Malaki 2:10).

Akizungumzia juu ya wakati wa utawala wa milenia Zekaria 14:9 anasema,

Naye Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa mmoja, na jina lake moja.” Kwa kifupi, Agano la Kale linasema kuna Mungu mmoja. Mara nyingi Biblia humwita Mungu “Mtakatifu Mmoja wa lsraeli” (Zaburi 71:22; 78:41; Isaya 1:4; 5:19; 5:24; 43:14, 15; 48:17).

Wala kamwe si “watakatifu wawill,” “watakatifu watatu” au “watakatifu wengi”. Anapofikiri juu ya jambo hili tutatambua kuwa Mungu Alitumia lugha yenye nguvu zaidi iwezekanavyo, iliyopo ili kuelezea umoja tu. Katika aya zilizotangulia za Maandiko ya Isaya, tunaona kuwa matumizi ya maneno na vifungu vya maneno kama vile “hapana, hapana mwingine, hapana aliye kama mimi hapana zaidi ya

mimi,peke yangu,” na “mmoja” Hakika, Mungu asingeweza kuweka wazi zaidi ya kuwa hakuna wingi wowote uliopo katka Uungu. Kwa kifupi, Agano la Kale

inathibitisha kuwa Mungu ni mmoja tu katika idadi.

AGANO JIPYA HUFUNDISHA YA KUWA KUNA MUNGU MMOJA TU

    Kwa kukazia Yesu alifundisha   Kumbukumbu la Torati 6:4  akiita amri ya kwanza kati ya zote (Marko 12:29-30). Agano jipya linaendelea kufundisha fundisho la Mungu mmoja na kwa uwazi inarudiarudia ujumbe ujumbe huu mara nyingi. 

 “.Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki”  [Warumi 3:30].

“….Hakuna Mungu ila mmoja tu:” (I Wakorintho 8;4)

“Lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu,aliye Baba”(1 Wakorintho 8:6).

“Bali,Mungu ni mmoja”(Wagalatia 3:20).

“..Mungu ni mmoja” (I Timotheo 2:5).

“Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote” (Waefeso4:6);

“Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vyema. Mashetani nao waamini na kutetemeka” (Yakobo2:19).

Tena, Biblia inamwita Mungu, “Mtakatifu Mmoja”           

[1 Yohana 2:20]. Kuna Kiti cha Enzi Kimoja Mbinguni na Mmoja ameketi juu ya kile kiti (Ufunuo 4:2). Siyo viti vitatu vya enzi au nafsi tatu za Mungu! Ni nani basi atakayeketi juu ya kile kiti cha Enzi kimoja?

Tunapata jibu kwenye Waebrania 1:8

“Lakini kwa habari ya Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele:..” Mwana (Yesu Kristo), atakaa juu ya Kiti Kimoja cha pekee Mbinguni. Yeye ataitwa Mungu na Kiti Chake cha Enzi ni cha milele na milele!

Na. Mwj. George

whatsapp/call: +255 782 044 449

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top